WATUMISHI WA SEKRETARIETI YA AJIRA WAMETAKIWA KUONGEZA
KASI NA UFANISI KATIKA KUENDESHA MCHAKATO WA AJIRA NCHINI
|
Watumishi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
wametakiwa kuongeza kasi katika kuendesha mchakato wa ajira pamoja na
kuzingatia maadili katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
Dkt. Laurean Ndumbaro amesema hayo wakati alipotembelea Ofisi za Sekretarieti
ya Ajira na kukutana na Menejimenti pamoja na Watumishi wa ofisi
hiyo ili kujifunza na kujionea namna Sekretarieti ya Ajira inavyofanya kazi
katika kutimiza majukumu iliyokabidhiwa.
“Ni vyema mkafanya kazi kwa kasi zaidi ili siku za
kuendesha mchakato wa ajira zipungue, na pia ni muhimu kuendelea kufuata
maadili ya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu ili mtu
anayeajiriwa awe ni yule mwenye sifa na vigezo stahili na si vinginevyo”
alisisitiza Dkt. Ndumbaro.
Aliongeza kuwa endapo watumishi watazingatia maadili ya
Utumishi wa Umma ipasavyo basi malalamiko ya upendeleo kutoka kwa wadau
yanaweza kupungua kama sio kuisha kabisa kwa kuwa anatambua fursa za
ajira ni chache na kila mwombaji angependa kupata fursa.
Mbali na hayo alihimiza juu ya umuhimu wa kuwa na vikao
vya pamoja baina Idara, Vitengo na Menejimenti kukutana kwa pamoja kila mara
ili kufanya kazi kwa ushikiano zaidi, kwa kuwa kila mtumishi atakuwa
anafahamu kinachoendelea ndani ya taasisi na mikakati iliyopo kwa lengo
la kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi.
Aidha, Katibu Mkuu huyo aliweza kupata maelezo ya kina ya
namna majukumu ya mchakato wa ajira yanavyotekelezwa na ofisi hiyo pamoja na
kujionea hatua kwa hatua namna mfumo wa kupokea maombi ya kazi kwa njia ya
Kielektroniki unavyofanya kazi kuanzia tangazo la kazi linapotolewa, mwombaji
wa fursa za ajira anavyojisajili na kuwasilisha maombi yake ya kazi na
taratibu nyingine zinavyofanyika hadi mchakato mzima wa ajira
kukamilika.
Ndumbaro alipongeza matumizi ya mfumo wa
kielektroniki unaotumiwa na taasisi hiyo kwa kuwa umeweza kusaidia kupunguza
baadhi ya malalamiko hususani ya kupotea kwa maombi ya kazi.
Aidha, alisema amepokea changamoto ambazo Sekretarieti ya
Ajira inakabiliana nazo na kuahidi kuangalia namna atakavyoweza kushirikiana
na taasisi hiyo katika kukabiliana nazo ili chombo hicho kiweze kutekeleza
majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Bw.
Xavier Daudi mbali na kutoa ufafanuzi wa namna chombo hicho kinavyofanya
kazi, alimshukuru Katibu Mkuu huyo kwa kuwatembelea na kuahidi utendaji wenye
tija zaidi ili kukidhi malengo.
Imetolewa na kitengo cha mawasiliano Tanzania.
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
29 Januari, 2016
|